Young Africans Hamsini kwa Hamsini Kutinga Makundi CAF
Kocha Mkuu wa timu ya Young Africans Nasreddine Nabi amesema timu yake bado inanafasi ya kutinga hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kocha huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari za michezo mara baada ya mchezo huo uliopigwa kwa Makapa saa 10:00 jioni. Nabi alisema timu yake imecheza vizuri katika safu ya ulinzi kwa dakika zote 90 lakini haikufanikiwa kutengeneza nafasi nyingi za magoli kutokana na aina ya mbinu ya kujilinda walioingia nayo wapinzani wao.
Aliongeza kuwa licha ya kushindwa kuipenya safu ya ulinzi ya Club Africain kwenye mchezo huo muhimu kwao, bado timu ya Young Africans iliweza kutengeneza nafasi chache ambazo kama wachezaji wengeongeza umakini wangepata matokeo.
Hata hivyo, kocha Nabi alikipongeza kikosi chake kwa kutoruhusu goli nyumbani na kusema kuwa watakwenda kupambana kutafuta matokeo kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa ugenini Novemba 9, 2022. Aliongeza akidai kuwa bado kikosi chake kina uwezo wa kusonga mbele kwani kutokana na matokeo ya 0-0 mpaka sasa hakuna mwenye uhakika kwa asilimia 100 kuwa atashinda; kila mmoja ana 50% ya kuingia makundi.
Kocha Nabi alisema mpira wa miguu ni mchezo unaotegemea mmoja akosee ili mwingine atumie makosa hayo kupata matokeo hivyo, watarekebisha makosa yaliyojitokeza na kwenda kutafuta matokeo ugenini kwani katika soka lolote linawezekana pasipo kujali upo nyumbani ama ugenini.
Naye kocha wa Club Africain, Bertrand Marchand alikipongeza kikosi chake kwa kufanikiwa kutoruhusu hata goli moja, hali hiyo kwa upande wao inaahweni kwa kuwa wanaamini nyumbani watakwenda kutafuta matokeo chanya. Alisema mchezo wa kwanza umekwisha wanashukuru, sasa kazi kubwa iliyobaki ni kwenda kuitumia vyema ardhi ya nyumbani. Aliongeza kuwa Young Africans ni timu nzuri na kubwa lakini wao watakwenda kujipanga zaidi ili waweze kushinda na kufanikiwa kuingia hatua ya makundi; hatua ambayo kila timu inahitaji kufika.
Mchezo uliopigwa kwa Mkapa ulimalizika kwa suluhu ya 0-0 na sasa timu hizo zinatarajia kucheza mechi ya marudiano mnamo Novemba 9, 2022 nchini Tunisia ambapo mshindi wa jumla ndiye atakayeingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.