Young Africans, Tabora United Kukipiga Azam Complex Chamazi

Mchezo wa tatu hatua ya robo fainali mashindano ya CRDB Bank Federation Cup inatarajia kukutanisha miamba miwili ya ligi kuu ya NBC Young Africans dhidi ya Tabora United, mchezo utakao pigwa uwanja wa Azam Complex Chamazi majira ya saa 2:30 usiku.

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi alisema hautakuwa mchezo rahisi, na kwamba wanautazama mchezo huo kwa utofauti na mechi za awali.

Alisema mechi ya robo fainali ya kombe la Shirikisho inaweza kuwa na mabadiliko makubwa ya kiufundi kulingana na aina ya mazoezi waliyofanya jana jioni.

“Wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo, tumefanya maandalizi ya kutosha, suala la Pacome (Zouzoua) ameanza kufanya mazoezi magumu na mtarajie kuona maendeleo yake endapo akipata nafasi ya kucheza walau kwa dakika chache,” alisema Gamondi.

Kwa upande wa kocha Msaidizi wa Tabora United Masoud Juma mwenyewe alisema wanafahamu umuhimu wa mechi za mtoano kwamba ni tofauti na mechi za ligi hivyo kila mmoja anahitaji matokeo ya tija kwake, alisema michezo ya mtoano inambinu tofauti hivyo watakwenda na mambo matatu muhimu ikiwemo kumuheshimu mpinzani wake, kutofanya makosa na kutocheza kwa kuhamaki mbele ya wapinzani wao.

“Tukiwa makini kwa mambo haya matatu ninaimani utakuwa mchezo mzuri, ukiangalia kwenye makaratasi unaona Tabora United tunaenda kufungwa kulingana na ubora wa mpinzani wetu lakini soka hakuna hilo jambo. Heshima yetu Kwa Young Africans ndio naamini itakuwa tiketi ya kuweza kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo, sisi tuko vizuri kuikabili timu yoyote ile bora hivyo tusubiri dakika 90″ alisema kocha.

Naye nahodha wa timu hiyo Said Mbatty alisema morali yao iko juu na kwamba wamekuwa wakitiana moyo mara zote kuutazama mchezo huo Kwa taswira ya kuonyesha ubora wao kwa wapenzi na mashabiki wa Tabora United.

“Tumejiandaa vizuri Kwa kuwa tunafahamu ubora wa timu tunayokwenda kukutana nayo, hivyo tumejiandaa kuyafanyia kazi maelekezo yote tuliyopewa na walimu wetu kwenye uwanja wa mazoezi”

Aidha nahodha huyo amewataka mashabiki wa Tabora United waendeleze imani Ile Ile ambayo wakonayo juu yao kwani imani yao ni kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo na hata kujikatia tiketi ya kucheza nusu Fainali.

Michezo mwingine ya robo fainali itakayo pigwa kesho ni ile itakayozikutanisha Ihefu FC na Mashujaa FC mapema kabisa majira ya saa 10:00 jioni uwanja wa Liti, na baadae kitapigwa Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani kati ya Coastal Union na Geita Gold FC majira ya saa 12:15 jioni.