Young Africans, Ruvu Shooting Zatambina Kuelekea Mchezo Wao Kwa Mkapa

Timu za  Young Africans na Ruvu Shooting zimetambiana kuelekea katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakao chezwa Juni 17, 2021 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Tambo hizo na majigambo yalitolewa na makocha pamoja na manahodha wa timu hizo walipokuwa kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi na waandishi wa habari za michezo ambapo kila mmoja alijigamba kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

Mchezo huo wa marudiano unakwenda kupigwa ikiwa mwenyeji ni Ruvu Shooting ambaye katika mchezo huo ataingia akiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 2-1 kwenye mchezo wao wa awali uliopigwa desemba 6, 2020 hapo hapo kwa Benjamin Mkapa; Young Africans ndiye aliyekuwa mwenyeji kwenye mchezo huo wa awali.

Kocha msaidizi wa kikosi cha Ruvu Shooting Rajabu Mohamed amesema kuwa wamejiandaa vya kutosha kuelekea mchezo huo na kwamba wanawaheshimu Young Africans kuwa ni timu kongwe na wazoefu lakini hiyo sio sababu ya wao kupoteza mchezo huo muhimu kwao.

Kocha alisema kuwa  kikosi chao kipo salama isipokuwa watawakosa baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi na wengine wanao tumikia adhabu ya kadi nyekundu, ambapo aliwataja majeruhi hao ni Musa, Renatus Kisase  na Juma Nyoso ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu lakini pia goli kipa wao namba moja pia hatakuwepo.

Nahodha wa kikosi hicho cha Ruvu Shooting, Renatus Ambros kwa upande wao wachezaji alisema kuwa wamejiandaa kwenda kufanya yale waliyoagizwa na makocha wao na lengo kubwa zaidi ni kupata alama tatu.

Kwa upande wa kocha msaidizi  wa Young Africans, Razack Siwa amesema kuwa wanakwenda kuendeleza rekodi yao ya kuwapiga Ruvu kwani anaamini kikosi chake kiko vizuri kutokana na mazoezi waliyokuwa wakiendelea kuyafanya kwa kipindi chote cha mapuziko.

Naye nahodha msaidizi wa Young Africans Ramadhani Kabwili alieleza kuwa wapo vizuri na kwamba wana morali kubwa ya kwenda kushinda mechi hiyo, lakini pia wataingia na tahadhari kutokana na timu ya Ruvu Shooting kuwa chini ya mwalimu mzuri lakini pia anayeijua vizuri Young Africans.

Timu hizi zinakutana ikiwa kila mmoja ana malengo yake; wakati Young Africans aliye nafasi ya pili akiwa amejibebea alama 61 mipango mikakati anahitaji kuendelea kupambana kugombania ubingwa, Ruvu Shooting yeye anaingia kwenye mchezo huo akiwa nafasi ya kumi na alama zake 37 huku akilenga kujikwamua kwenye hatari ya kushoka daraja ama kungojea micho ya mtaani ili kupata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Bara. Hivyo kushinda kwake katika mchezo huo atakuwa kajiweka mahali pazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.