Young Africans Yaishusha Azam FC Kileleni Ligi Kuu Bara

Timu ya Young Africans imefanikiwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuichapa mabao 2-0 timu ya Dodoma Jiji kwenye mchezo uliopigwa Novemba 22, 2022 majira ya saa 10:00 katika uwanja wa Liti uliopo mjini Singida.

Mchezo huo baina ya timu hizo ulikuwa mkali ambapo timu zote zilikuwa na hamu ya kupata alama tatu. Dodoma jiji walifanikiwa kumiliki mchezo kwa asilimia 51, huku Young Africans wakipata umiliki wa asilimia 49 licha ya kuibuka na ushindi.

Mabao mawili ya Fiston Mayele (41, 67) yalitosha kuipa ushindi timu hiyo ya wananchi kwani mpaka dakika 90 zinatamatika Young Africans wanatoka kifua mbele kwa mabao 2-0, na hivyo kuwafanya warejee kileleni mwa Ligi Kuu Bara.

Wachezaji wawili, mmoja kutoka kila  timu walipata nafasi ya kuzungumza baada ya mcheo huo kumalizika; Fiston Kalala Mayele alisema kuwa wao wamefurahi kupata matokeo ugenini na hasa yeye kuweza kufanga magoli mawili na kumfanya kufikisha mabao 8 huku akifunga magoli 5 kwenye mechi mbili. Aliweka bayana kuwa magoli hayo aliyofunga ni zawadi kwa Mkewe pamoja na mwanaye aliyempata siku za karibuni.

Kwa upande wa nahodha wa Dodoma Jiji, Emmanuel Joseph  Martin alisema kuwa walizidiwa kidogo na wakalazimishwa kufanya makosa yaliyopelekea wao kupoteza mchezo huo. Martin aliongeza kuwa kocha na benchi la ufundi wamekwisha yaona makosa yalijitokeza hivyo wao kama wachezaji wapo tayari kupokea maelekezo kutoka kwa walimu ili waweze kushinda michezo miwili iliyo mbele yao.

Matokeo ya Mchezo huo yanaifanya Young Africans kufikisha alama 29 sawa na Azam FC huku wakiongoza ligi kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa. Azam FC anafaida ya magoli +7 wakati Young Africans wao wana faida ya magoli +15.