Young Africans Yarejea Kileleni Ligi Kuu Bara
Timu ya Young Africans imefanikiwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliochezwa Novemba13, 2022 katika dimba la CCM Kirumba Jijini Mwanza mnamo majira ya saa 10:00 jioni.
Katika mchezo huo Kagera Sugar ndio walikuwa wa moto zaidi licha ya kushindwa kupata matokeo. Mlinda mlango wa Young Africans Djigui Diarra alikuwa kikwazo kwa timu hiyo kupata magoli. Goli pekee la Clement Mzinze lililopatikana dakika ya 19 kipindi cha kwanza liliwafanya Young Africans kuondoka na ushindi uliowawezesha kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi.
Kagera Sugar walifanikiwa kupata mkwaju wa penati ambao haukuweza kuzaa bao, jambo lililowapatia nguvu wachezaji wa Young Africans walioongeza kujiamini zaidi kwenye mchezo huku wapinzani wao wakivunjika moyo japokuwa hawakukata tamaa na badala yake kuendeleza mambano yalioambatana na msako mkali mpaka dakika 90.
Kocha Mecky Mexime baada ya mchezo huo alisema kuwa kikosi chake kilicheza vizuri na kuishika mechi hiyo lakini walikosa bahati na umakini wa kumalizia nafasi nyingi walizozitengeneza. Mexime alimpongeza kocha wa Young Africans Nasreddine Nabi kwa mpango kazi alioingia nao kwani umeweza kumlipa. Vile vile, alitoa pongezi kwa Nabi kwa kuiwezesha timu yake kutinga hatua ya Makundi Shirikisho pamoja na kupata ushindi.
Kwa upande wake Nasreddine Nabi wa Young Africans yeye aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupata ushindi huo akidai kuwa ulikuwa ni muhimu kwao ili kurudi katika nafasi yao kwenye msimamo wa Ligi Kuu. Alieleza licha ya uchuvu wa safari waliokuwa nao bado isingekuwa sababu ya kupoteza mchezo huo ndo maana aliamua kuwapomzisha baadhi ya nyota wake na kuanza na wachezaji ambao mara nyingi hukosa nafasi ya kuanza.
Hata hivyo, kocha Nabi naye alikipongeza pia kikosi cha Kagera Sugar kwa mchezo mzuri kiliouonesha na kwamba anakiri kuwa Kagera walikuwa bora zaidi kwenye michezo huo licha ya matokeo kutokuwa upande wao.
Katika mchezo mwingine uliopigwa majira ya saa 8:00 kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, timu ya Coastal Union iliilazimisha sare ya bao 2-2 Mbeya City kwenye mchezo ulikuwa na ushindani mkali. Coastal Union ndiyo waliotangulia kupata bao kwenye dakika ya 24 kupitia kwa Greyson Gwalala kabla ya Sixtus Sabilo kusawazisha dakika 39 ya mchezo na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko kwa sare ya 1-1.
Katika dakika ya 70 ya mchezo Hamad Majimengi aliwapachikia bao la pili Wagosi wa Kaya, na baadaye Sixtus Sabilo akachomoa tena kwenye dakika ya 79 kwa mkwaju wa penati; hivyo kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 2-2.
Matokeo hayo yanaifanya Costal Union kujikusanyia alama 4 kwenye mechi mbili za ugenini na kufikisha alama 12 huku Mbeya City wao wakiwa juu ya baada kujikusanyia alama 16.