Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

MSHAMBULIAJI wa timu ya Alliance ya Mwanza, Dickson Ambundo, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
Ambundo alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, mshambuliaji Ayoub Lyanga wa Coastal Union ya Tanga na kipa Juma Kaseja wa KMC ya Dar es Salaam, alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mwezi huo wa Januari, Alliance ilicheza michezo mitano, ambapo Ambundo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake kupata pointi 11 ikishinda michezo mitatu na kutoka sare miwili, huku mshambuliaji huyo akifunga mabao matatu na timu hiyo kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya tisa katika msimamo wa ligi inayoshirikisha timu 20.

Kwa upande wa Kaseja alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timu ya KMC kwa mwezi huo, ambapo timu yake ilicheza michezo minne ikishinda yote na kujikusanyia pointi 12 na kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya tatu, ambapo Kaseja aliruhusu bao katika mchezo mmoja dhidi ya Coastal Union ambao KMC ilishinda mabao 5-2, wakati Lyanga alionesha uwezo mkubwa katika michezo ya Coastal Union na kuwa tumaini katika ufungaji ikiwa ni pamoja na kupachika nyavuni mabao matatu.

Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha wa KMC, Etiene Ndayiragije kuwa Kocha Bora wa mwezi Januari akiwashinda Kocha Mkuu wa Alliance, Malale Hamsini na Kocha Mkuu wa Biashara United, Amri Said alioingia nao fainali.

Ndayiragije aliiongoza timu yake katika michezo minne iliyocheza, ambayo KMC ilishinda michezo yote na kuvuna pointi 12 na kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Kwa upande wa Malale yeye aliiongoza timu yake katika michezo mitano ikishinda mitatu na kutoka sare miwili ikipanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya tisa katika msimamo, wakati Amri Said kwa mwezi huo timu yake ilicheza michezo sita, ikishinda mitatu, sare mmoj na kupoteza miwili hivyo kupanda kutoka nafasi ya 20 hadi ya 18 katika msimamo.

TFF ina utaratibu wa kuwazadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kategori mbalimbali.

Washindi wengine wa tuzo hiyo kwa msimu huu na miezi yao katika ni Meddie Kagere wa Simba (Agosti), Eliud Ambokile wa Mbeya City (Septemba), Emmanuel Okwi wa Simba (Oktoba), mwezi Novemba na Desemba alishinda Heritier Makambo wa Yanga.

Kwa upande wa makocha walioshinda tuzo hizo kwa msimu huu ni Amri Said wakati huo akiwa Mbao FC (Agosti), Mwinyi Zahera wa Yanga (Septemba), Hans Pluijm wa Azam (Oktoba), wakati Novemba na Desemba alishinda Mwinyi Zahera wa Yanga.

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.