Kocha wa timu ya Taifa ya Wanawake U20 (Tanzanite Queens), Bakari Shime amesema makosa waliyofanya wachezaji wake yalisababisha wapoteze mchezo dhidi ya Canada katika fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazofanyika nchini Poland.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo waliopoteza kwa mabao 6-0, Shime amesema mabao mawili ya haraka waliyofungwa yaliwatoa mchezoni na kupoteza kujiamini.
Shime alisema kipindi cha pili, walijipanga kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao lakini bahati mbaya wakafanya makosa kwa kuwaruhusu wapinzani kumiliki mpira karibu na goli hali iliyowapa faida ya kupata mabao mawili ya haraka haraka ambayo yakawatoa kwenye mchezo.
Alisema pamoja na ugumu wa matokeo katika hatua ya makundi lakini mashindano hayo yamekuwa moja ya sehemu ya kujifunza na wamejua kuwa kiwango cha shindano kilikuwa kinahitaji kuwa na uwezo wa aina gani ili waweze kucheza.


