CAF yakagua miundombinu ya AFCON 2027
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya ukaguzi wa miundombinu inayoandaliwa kwa ajili ya Fainali za AFCON zitakazofanyika Juni 2027.
Wakaguzi hao walioongozwa na Mkuu wa Mashindano wa CAF, Khaled Nassar waliwasili jijini Dar es Salaam tarehe 2 Septemba ambapo walifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.
Maeneo hayo ni Uwanja wa Benjamin Mkapa (Dar es Salaam), Uwanja wa Arusha, na Uwanja wa Fumba (Zanzibar). Kwa upande wa Tanzania, viwanja hivyo ndivyo vilivyopangwa kutumika kwenye fainali hizo.
Maeneo mengine yaliyofanyiwa ukaguzi ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), viwanja vya mazoezi kwa ajili ya michuano hiyo kwenye miji yote mitatu.
Vilevile wakaguzi hao walikagua hospitali, hoteli, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara kuelekea kwenye viwanja vya mechi.
Ukaguzi wa CAF ulianzia nchini Kenya, na Uganda ambapo nchi hizo pamoja na Tanzania ndiyo wenyeji wa fainali hizo na Pamoja AFCON 2027 zitakazoanza tarehe 19 Juni hadi 17 Julai.
Akizungumzia ukaguzi huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema:
“Bado tuko ndani ya malengo tuliyojiwekea ya kuhakikisha tunakamilisha maandalizi yote kwa wakati ili tuwe na mashindano mazuri mwakani.
“Kiujumla wakaguzi wameridhishwa na kasi tunayoenda nayo, tunasubiri tathimini ya mwisho watakayotoa baada ya ziara kumalizika.”


