FIFA, TFF zawapiga msasa maofisa Wanawake

    Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeendelea kuunga mkono juhudi za kukuza na kuimarisha mpira wa miguu wanawake nchini.

    FIFA kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) waliendesha warsha maalumu ya siku tatu iliyofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 27 hadi 29 Agosti.

    Warsha hiyo ililenga kuwaongezea uwezo viongozi na wadau wa mpira wa miguu, hasa wanaohusika na usimamizi na maendeleo ya mpira wa miguu wa wanawake, ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na kuchangia ukuaji wa mchezo huo nchini.

    Katika siku hizo tatu, washiriki walipata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuendesha, kusimamia na kuendeleza mpira wa miguu wa wanawake, huku msisitizo ukiwekwa katika uongozi bora, mipango ya maendeleo, usimamizi wa timu, mashindano pamoja na namna ya kuongeza ushiriki wa wanawake.

    Share.