Mshambuliaji wa Tanzania, Clara Luvanga, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kike ghali zaidi kuwahi kusajiliwa duniani, kufuatia uhamisho wake kutoka Al-Nassr ya Saudi Arabia kwenda Washington Spirit ya Marekani.
Clara amejiunga na klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake nchini Marekani (NWSL) kwa ada ya uhamisho inayoripotiwa kufikia dola milioni 2.3 za Marekani (zaidi ya Tsh. 5.9 bilioni).
Ada hiyo inamfanya Luvanga kushika nafasi ya kwanza katika historia ya soko la uhamisho wa wachezaji wa kike duniani, akivunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Lizbeth Ovalle wa Mexico, ambaye uhamisho wake ulikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 1.5 (zaidi ya Tsh. 3.9 bilioni).
Baada ya rekodi hiyo Clara anafuatiwa na Lizbeth Ovalle (dola milioni 1.5), Olivia Smith (dola milioni 1.36), Alyssa Thompson (dola milioni 1.343), Grace Geyoro (dola milioni 1.34) na Naomi Girma (dola milioni 1.1).
Uhamisho wa Clara unaonyesha kuendelea kukua kwa uwekezaji wa kifedha katika soka la wanawake duniani, huku klabu zikiwa tayari kutumia fedha kubwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa.


