Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameliomba Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kutunga kanuni kwa wanaowania kuongoza michezo nchini kuwa na elimu ya uongozi.
Rais Karia alitoa maombi hayo wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti vya mafunzo ya juu ya Uongozi na Usimamizi wa Michezo (Advanced Sport Management Course) awamu ya tatu ya mafunzo yanayotolewa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) iliyofanyika Makao Makuu ya TFF, Ilala jijini Dar es Salaam.
Alimuomba Mwenyekiti wa BMT, Leodger Tenga kuona jinsi ya kuweka kanuni zitakazotaka wanaowania uongozi wa michezo wapitie kozi za uongozi wa michezo ili kuwawezesha kuihudumia michezo kwa weledi zaidi.
Kwa upande wake, Tenga amelipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kutoa washiriki wengi katika kozi hiyo na kuyataka mashirikisho mengine ya michezo kuiga mfano huo, huku akitoa ahadi ya kuzungumza na watendaji wake wa BMT kufuata nyayo hizo.


