Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) Simba Queens na Yanga Princess wamezidi kuchanja mbuga baada ya kushinda mechi zao za raundi ya pili zilizochezwa leo.
Simba Queens waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate Princess katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Bao pekee lililoipa ushindi Simba Queens lilipatikana baada ya Felister Mauki kujifunga dakika ya 56 na kuwapa pointi tatu mabingwa watetezi.
Yanga Princess wenyewe walikusanya pointi tatu ugenini dhidi ya Geita Queens baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita.
Mabao ya Yanga Princess katika mechi hiyo yalifungwa na Rehema Ramadhan dakika ya 76 na Mesaya Tanga dakika ya 90.
Mechi nyingine zilizopigwa leo, JKT Queens waliendeleza ubabe kwenye mechi za ugenini baada ya kupata ushindi mwingine wa mabao 2-0 dhidi ya Bunda Girls.
Ceasiaa Queens wakiwa nyumbani wameweka heshima kwa kuichapa Bunda Queens mabao 4-2, huku Tausi wakipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Alliance Girls.
Mashujaa Queens walifanikiwa kukusanya pointi tatu wakiwa ugenini baada ya kuichapa Kilimanjaro Wonders kwa mabao 2-1.


