Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanaume U20 (Ngorongoro Heroes), Mario Rivera, ameridhishwa na maendeleo ya kikosi chake licha ya kupoteza kwenye mechi mbili za kirafiki dhidi ya Misri.
Rivera amesema mechi ya mwisho ilikuwa bora zaidi kwa upande wa Ngorongoro Heroes, akieleza kuwa wachezaji walionesha ujasiri wa kumiliki mpira, kucheza kwa kushirikiana na kutengeneza mashambulizi kupitia muunganiko mzuri wa pasi.
Kocha huyo ameeleza kuwa makosa mawili ndiyo yaliyochangia timu kuruhusu mabao 2-0, huku akilitaja tukio lililosababisha bao la kwanza ni kukosa uzoefu na kufanya maamuzi yasiyo sahihi.
Rivera amesema wakati wa tukio hilo timu ilikuwa na wachezaji 10 baada ya mchezaji mmoja kuumia na kutoka nje kwa takribani dakika moja kwa mujibu wa kanuni.
Ameeleza kuwa katika kipindi hicho wachezaji walishindwa kusoma vizuri hali ya mechi na kufanya pasi ya ndani iliyokuwa na hatari kubwa karibu na lango lao, badala ya kucheza mpira kuelekea eneo salama.
“Unapokuwa na wachezaji 10, unatakiwa kuwa na busara zaidi na kucheza mpira mbali na lango lako. Pasi tuliyocheza ilikuwa hatarishi, tukapoteza mpira na kuruhusu bao,” amesema Rivera.
Licha ya hayo Rivera amesema ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji, akibainisha kuwa baadhi yao wameonesha maendeleo makubwa katika kipindi hiki cha maandalizi.
Rivera amesisitiza kuwa licha ya matokeo ya mechi hiyo, maboresho yaliyoonekana katika uchezaji ni jambo la kutia moyo katika hatua hii ya maandalizi ya timu hiyo kujiandaa na AFCON 2027.


