Kocha wa Timu ya Taifa ya Wavulana U17 (Serengeti Boys), Elieneza Nsanganzelu amesema mechi ya mwisho dhidi ya Jamhuri ya Ireland ndio iliyobeba matumaini yao kwenye Kombe Dunia linaloendelea Qatar.
Serengeti Boys imesalia na mchezo mmoja wa hatua ya makundi ambao ndio wenye tiketi ya kikosi hicho kusonga hatua ya mtoano.
Nsanganzelu amesema anaamini kwenye mechi hiyo ya mwisho watapata matokeo mazuri kutokana na kiwango bora walichoonesha dhidi ya Brazil.
Alisema mechi dhidi ya Brazil ilikuwa ngumu lakini walionesha kiwango bora licha ya kupoteza baada ya kufanya kosa ambalo wapinzani wao walilitumia kuwaadhibu lakini sasa nguvu zote watazielekeza kwenye mechi ijayo.
Serengeti Boys ipo kwenye Kundi I wakiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costa Rica kwenye mechi wa kwanza na kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Brazil kwenye mechi ya pili.


