Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeidhinisha lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi za shirikisho hilo baada ya kufanya mabadiliko madogo katika Katiba ya CAF.
Rais wa CAF Dk. Patrice Motsepe ametangaza rasmi kuwa Kiswahili ni lugha rasmi ya CAF baada ya kupigiwa kura nyingi za kishindo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 48 wa CAF uliofanyika Jijini Abuja, Nigeria.
Kufuatia uamuzi huo, Kiswahili kinaungana na lugha nyingine nne ambazo ni Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kireno kuwa lugha rasmi zinazotumika katika shughuli za CAF ikiwemo mikutano na matukio mbalimbali yanayoandaliwa na CAF.
Akitangaza uamuzi huo, Rais Motsepe ameipongeza Tanzania, Kenya na Uganda kwa kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya CAF na kwamba anaamini hiyo ni fursa muhimu kwa Afrika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambaye amemwakilisha Waziri wake, Paul Makonda katika mkutano huo, amesema Tanzania na Afrika Mashariki imepokea uamuzi huo wa CAF kwa heshima kubwa na itahakikisha inatumia fursa hiyo ipasavyo kukuza Kiswahili na utamaduni wa Mswahili.

Msigwa ambaye ameambatana na Balozi wa Tanzania Abuja, Nigeria Selestine Kakele na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia wameeleza furaha yao na shukrani zao za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia mchakato wa kuomba Kiswahili kuwa lugha rasmi ya CAF tangu miaka mitatu iliyopita jambo ambalo limefanikiwa.


