Raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) 2026/2027 unatarajiwa kuchezwa kesho Novemba 4, 2026 miamba 12 ya ligi hiyo wakishuka katika viwanja sita kuwania pointi tatu muhimu.

    Msimu wa TWPL ulionza kutimua vumbi Oktoba 28 2026 ulishuhudia timu za Simba Queens, Yanga Princess, Bunda Queens, JKT Queens, Mashujaa Queens na Alliance Girls wakiibuka na ushindi katika mechi zao za kwanza, kesho wataingia uwanjani kutaka kuendeleza ubabe wakati waliopoteza wakitaka kujiuliza.

    Katika mechi za kesho Kilimanjaro Wonders baada ya kupoteza mechi ya kwanza watajiuliza kwa Mashujaa Queens kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Bunda Girls watawakaribisha JKT Queens mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Karume mkoani Mara.

    Fountain Gate Princess watakutana na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba Queens kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Tausi FC waliopoteza mechi iliyopita watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kucheza na Alliance Girls.

    Timu ya Ceasiaa Queens watakuwa kwenye Uwanja wake wa Samora mjini Iringa wakivaana na Bunda Queens wakati Geita Queens watapepetana na Yanga Princess mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

    Share.