Twiga Stars yakamilisha maandalizi ya WAFCON
Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) inaendelea na matayarisho kwa ajili ya Fainali za WAFCON zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Julai 26 mwaka huu.
Twiga Stars iliyoweka kambi Karatu mkoani Arusha inatarajia kuanza safari ya kwenda Morocco wiki hii ili kucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kuanza Fainali hizo.
Akizungumza baada ya mazoezi ya mwisho, Kocha Mkuu mkuu wa timu hiyo Bakari Shime alisema matayarisho yao yamekwenda vizuri kwa kipindi chote cha kambi hiyo na tayari timu ina msingi mzuri na kilichobaki ni kupata mechi angalau mbili za kujipima nguvu.
Alisema ari ya wachezaji iko juu tayari kwa michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa upande wa mpira wa miguu wa wanawake.
“Ushindani ni mkubwa sana kwa wachezaji kila mmoja akiwa na matamanio ya kuwa sehemu ya Fainali hizo.
“Tumepanga kucheza mechi mbili za kirafiki tukiwa nchini Morocco. Tutacheza na Nigeria Julai 19 na mechi nyingine itakuwa dhidi ya Ghana au Mali,” alisema Shime.
Twiga Stars itacheza mechi ya kwanza ya WAFCON hatua ya makundi Julai 27 dhidi ya Afrika Kusini jijini Casablanca.


