Tiketi sasa kidijitali TFF

    Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua mfumo wa kidigitali utakaotumika katika ununuzi wa tiketi za kuingilia uwanjani.

    Mfumo huo utaanza kutumika kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba.

    Mechi hiyo ya ufunguzi rasmi wa mashindano ya TFF msimu wa 2026/2027 itachezwa Agosti 12 mwaka huu katika Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2:30 usiku.

    Akizungumzia mfumo huo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo alisema: “Mfumo utaanza kutumika leo Agosti 10, 2026 ambapo mashabiki na wadau wa soka watanunua tiketi za mechi ya Ngao ya Jamii kupitia tovuti ya www.tff-tickets.com.

    “Teknolojia inakua kwa kasi na huu ni wakati sahihi wa kuendana na mabadiliko hayo, kwani mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa tiketi za mechi husika kwa wakati na mahali popote ukiwa na simu janja.

    “Lakini pia itaondoa usumbufu wa kufata tiketi vituoni na kusubiri muda mrefu kupata huduma hiyo.”

    TFF litaendelea kufanya maboresho mbalimbali kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC na mashindano mengine ili thamani ya mpira wa miguu wa Tanzania izidi kupanda.

    Share.