Kozi ya VAR yaingia moduli ya tano
Kozi ya VAR (Video Assistant Referee) moduli ya tano imefunguliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Nassor Idrissa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kozi hiyo ni mwendelezo wa moduli zilizopita zenye lengo la kuwapa waamuzi ujuzi wa matumizi sahihi ya VAR ili kusaidia kupunguza makosa ya kibinadamu ikiwemo maamuzi sahihi ya mabao, penalti, kadi nyekundu na njano, eneo la kuotea na matukio mengine ambayo mwamuzi hakuyaona wakati wa mchezo.
Akizungumza wakati wa kufungua kozi hiyo, Makamu huyo wa Pili wa Rais wa TFF alisema:
“Malengo ya TFF ni kuona mpira wa miguu wa Tanzania unafikia viwango vya kimataifa, na ili tufike huko hatuna budi kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.”
Naye Mkufunzi wa kozi hiyo raia wa Ivory Coast, Nomandiez Doue aliwataka waamuzi kuzingatia mafunzo ya moduli ya tano ndio moduli muhimu zaidi ikilenga kuchunguza matukio yote ya kuotea na kuyatolea maamuzi, mazoezi ya VAR kwa vitendo na namna ya kufanya mawasiliano.
Waamuzi 20 wanashiriki kozi ambayo ipo chini ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ni Ramadhan Kayoko, Henry Sasii, Ahmed Arajiga, Nasir Siyah, Tatu Malogo, Amina Kyando, Mohamed Simba, Alex Pangras na Abdallah Mwinyimkuu.
Wengine ni Ester Ntandu, Frank Komba, Kassim Mpanga, Ally Rajab, Hamdan Ally, Mohammed Mkono, Janeth Balama, Glory Tesha, Zawadi Yusuph, Siraji Mkwaju na Shabani Musa
Kozi ya VAR moduli ya tano imeanza leo Julai 21, 2026 na itamalizika Julai 26, 2026.


