Twiga Stars waisubiri kwa hamu Burkina Faso
Twiga Stars imejidhatiti vyema kwa ajili ya mechi yake pili Fainali za Afrika kwa Wanawake (WAFCON) dhidi ya Burkina Faso.
Uwanja wa Labri Zaouli ulioko Casablanca ndiyo utakuwa mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa Julai 31, 2026 kuanzia saa 5 kamili usiku.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari, Kocha wa timu hiyo, Bakari Shime alisema licha ya ugumu wanaotarajia kukutana nao wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.
“Burkina Faso ni timu nzuri na tunawaheshimu. Tumewaona kwenye mechi yao ya kwanza, hivyo tumefanyia kazi mambo muhimu na tupo tayari kuwakabili,” alisema Shime.
Naye Nahodha wa Twiga, Opah Clement alisema Ari ipo juu kwa upande wao na kuwa wanajua faida ya kushinda ili wafikie malengo waliyojiwekea.
Lengo la timu hiyo kwa mujibu wa Kocha Shime ni kufika nusu fainali, nafasi ambayo itawapa tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2027.
Twiga Stars itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi ya kwanza kwenye Fainali hizo dhidi ya Afrika Kusini.


