What's Hot

    Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeanzisha utaratibu wa kuwakutanisha mashabiki wa soka nchini na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) uliopewa jina la Mashabiki Day.

    Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa TFF, Cliford Mario Ndimbo amesema siku hiyo itakuwa maalum kwa msahabiki kupata nafasi ya kuhudhuria mazoezi, wataruhusiwa kupiga picha na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

    Alisema kwa mujibu wa ratiba ya Taifa Stars tukio hilo litafanyika Septemba 23, 2026, wakati timu hiyo inatarajiwa kuingia kambini kesho na kuanza mazoezi siku hiyo kujiandaa na michezo miwili ya kuwania kufuzu fainali za AFCON 2027 na mmoja wa kirafiki dhidi ya Ghana.

    Ndimbo alisema waandishi wa habari nao wametengewa siku ya Jumatatu ya Septemba 21 ambapo wataruhusiwa kufanya mahojiano mbalimbali na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

    Mbali na Taifa Stars, Ndimbo pia amezungumzia programu za timu mbalimbali za Taifa, ambapo timu ya FUTSAL inatarajiwa kwenda nchini Morocco kushiriki mashindano ya AFCON 2026 zitakazofanyika kuanzia Oktoba 12 mpaka 21 mwaka huu.

    Kwa upande wa timu ya Taifa ya Beach Soccer, inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kuwania kufuzu fainali za AFCON 2027 dhidi ya Msumbiji mchezo wa kwanza ukichezwa Oktoba 11 jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana mjini Maputo kati ya Oktoba 16 na 18 mwaka huu.

    Ndimbo alisema timu ya Taifa ya Wavulana U17 (Serengeti Boys) ipo kambini ikiendelea na maandalizi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.

    Alisema timu ya Taifa ya Wanawake inayowania kufuzu michuano ya Olimpiki 2028 itakayofanyika Los Angels, Marekani, inatarajiwa kucheza michezo miwili dhidi ya Botswana ambapo mchezo wa kwanza utachezwa Oktoba 9 wakiwa ugenini na kurudiana jijini Dar es Salaam Oktoba 13 mwaka huu.

    Ndimbo alisema timu ya Taifa ya wanaume U23, wanaripoti kambini leo na kuanza mazoezi uwanja Gymkhana kujiandaa na michezo miwili ya kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Kenya, ambapo mchezo wa kwanza utachezwa ugenini Septemba 28 na kurudiana Oktoba 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

    Share.