Makocha Wanawake kukuza vipaji
Semina maalumu ya makocha wanawake imefanyika leo jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo katika kutambua, kulea na kukuza vipaji vya watoto wenye umri kuanzia miaka sita hadi 14.
Makocha wanawake kutoka maeneo tofauti, wameshiriki semina hiyo iliyowaongezea uelewa kuhusu namna bora ya kutambua vipaji vya watoto katika hatua za awali.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na Mtambuzi wa Vipaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Gideon Ngereza ambaye amesisitiza umuhimu wa kuwa na makocha wenye uelewa na weledi wa kutosha katika kuwasaidia watoto wenye vipaji kuanza safari yao katika mazingira sahihi.
Kupitia semina hiyo, makocha wanawake wamejifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za kutambua vipaji.
Makocha hao wanatarajiwa kuwa mabalozi muhimu katika utafutaji na ukuzaji wa vipaji vya watoto, hususan katika ngazi za chini ambako vipaji vingi huanza kuonekana.
Umuhimu wa kuwaandaa makocha katika eneo hili unatokana na ukweli kuwa umri wa miaka sita hadi 14 ni kipindi muhimu katika maendeleo ya mtoto kisoka.

Makocha wenye ujuzi wanaweza kusaidia kuhakikisha watoto wanapata msingi mzuri wa kiufundi, nidhamu, uelewa wa mchezo na mazingira yanayowapa nafasi ya kuendelea kukua.


