Timu ya Taifa ya Wanawake U20 (Tanzanite Queens) inatarajiwa kumalizana kibabe na Canada katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazofanyika nchini Poland.

    Kocha wa Tanzanite Queens, Bakari Shime amesema wachezaji wake wanaingia katika mchezo huo wakiwa na lengo moja tu la kusaka ushindi ili kuweza kusonga mbele hatua inayofuata.

    Shime amesema nafasi ya kusonga mbele bado ipo na wachezaji wana morali kuelekea mchezo huo na wamewasoma wapinzani wao na kufanyia mazoezi jinsi ya kuwazuia na kuwashambulia wanapokuwa na mpira, hivyo watapambana kupata matokeo mazuri.

    Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Nahodha wa Tanzanite Queens, Jamila Rajabu amesema wanaingia katika mchezo wa kesho kurekebisha makosa waliyofanya katika michezo iliyopita, wataingia mchezoni kwa heshima kwani wanaamini utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kushinda.

    Naye Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Nassor Idrissa amesema pamoja na Tanzanite Queens kupoteza michezo miwili iliypita lakini bado nafasi ya kufanya vizuri ipo.

    Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF na Mkuu wa Msafara wa Tanzanite Queens, Debora Mkemwa amesema haijaisha mpaka iishe, wanawaamini sana, Watanzania wamewatanguliza mbele na wao wapo nyuma yao, yote yanawezekana.

    Share.