CAF yaridhishwa maandalizi AFCON 2027
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kupitia Rais wake Patrice Motsepe limeridhishwa na maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) nchini Tanzania.
Rais Motsepe akiambatana na viongozi wengine wa CAF waliwasili nchini Septemba 17, 2026 na kukagua maendeleo ya miundombinu.
Pia walijadili mikakati mbalimbali pamoja na viongozi wa Kamati ya Maandalizi (LOC) ya Tanzania kuhusu fainali hizo.
Alisema anajivunia juhudi zinazofanywa nchini Tanzania kwa ajili ya fainali za AFCON 2027, huku akiwataka Watanzania na Serikali kuendelea na maaandalizi ikiwa imesalia miezi tisa kabla ya fainali hizo kuanza kutimua vumbi.
“Tunatakiwa kujiamini wenyewe kama Tanzania, kama Afrika na kama Afrika Mashariki kuwa kwa pamoja tunaweza kishirikiana kufanya kitu bora,” alisema Motsepe.
Alisema utayari wa Tanzania unathibitisha kuwa fainali hizo zitafanyika kwa ufanisi mkubwa hapo mwakani.
Alisema changamoto zozote zinazojiyokeza ni sehemu ya kuwa na fainali bora zaidi na kuwa CAF inalenga kuhakikisha nchi hizo (Tanzania, Kenya na Uganda) zinafikia malengo yake katika kufanikisha matayarisho hayo.
Rais huyo ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania pamoja na wadau wengine kwa ushirikiano mkubwa na Shirikisho hilo kwenye matayarisho.
Tanzania, Kenya na Uganda ni wenyeji wa mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.


