Mwenyekiti wa Chama Cha Soka la Wanawake Tanzania, Somoe Ng’itu ameutabiria msimu mpya wa Ligi ya Wanawake Tanzania (TWPL) 2026/27 kuwa utakuwa msimu bora zaidi kuliko iliyopita.
Somoe ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya TFF, amesema anataraji kuongezeka kwa mvuto na ushindani mkubwa msimu huu kutokana na matayarisho ambayo timu zimefanya sambamba na kukua kwa ligi hiyo kila msimu.
“Tumetembelea kila timu kuangalia maandalizi yao na hakika kwa kiasi kikubwa tumejiridhisha na matayarisho yao, yataleta ushindani mkubwa sana,” alisema Somoe.
Aidha alieleza tafsiri ndogo ya ushindani huo pia ulionekana kwa baadhi ya timu zilizobahatika kucheza mechi tatu za Ngao ya Jamii 2026 ambapo ni taswira ya ushindani utakaopatikana miongoni mwa timu nyingi msimu huo.
Katika hatua nyingine aligusia kukua kwa ligi hiyo ni pamoja na wadau kuendelea kuziunga mkono mechi za zake kwa kujitokeza viwanjani.
Ligi hiyo inatarajia kuanza kutimua vumbi Oktoba 28, 2026 kwa mechi za mzunguko wa kwanza huku timu 12 zikitoana jasho kusaka ubingwa.


