Tanzanite yabakiza matumaini kwa Canada

     

    Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens) bado haijapoteza matumaini ya kuvuka hatua ya makundi ya Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Poland.

     

    Tanzanite Queens imepoteza mechi mbili mfululizo mbele ya Brazil na England, na imebakiza moja dhidi ya Canada katika hatua ya makundi.

     

    Katika mechi ya pili iliyochezwa Septemba 8 dhidi ya England, Tanzanite ilifungwa mabao 5-1, lakini bado ina nafasi ya kusonga mbele endapo itashinda mechi hiyo ya Septemba 11.

     

    Akizungumza baada ya mechi, Kocha Mkuu Bakari Shime alisema licha ya kupoteza amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake na mabadiliko aliyoyaona kulinganisha na mechi ya kwanza hasa wachezaji wake kucheza kwa kufuata maelekezo waliyoyafanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi.

     

    “Tumefungwa kwa kuzidiwa ubora na wapinzani wetu, lakini wasichana leo wamefuata asilimia 100 ya maelekezo tuliyofanyia kazi mazoezini. Hiyo inanipa matumaini ya kufanya bora zaidi kwenye mechi ya mwisho,” alisema Shime.

     

    Aliongeza kuwa mechi ya mwisho bado ni muhimu

    kwao endapo watapata pointi tatu mbele ya Canada.

     

    Brazil ndiyo kinara wa kundi hilo baada ya kushinda mechi zote mbili, ikifuatiwa na England yenye pointi nne, huku Canada ikiwa na pointi moja. Tanzanite haina pointi yoyote.

    Share.