Nyota wa Tanzania, Clara Luvanga ameandika historia mpya baada ya kujiunga na klabu ya Washington Spirit inayoshiriki Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake nchini Marekani (NWSL).
Usajili huo wa miaka minne ambao utamweka katika klabu hiyo hadi mwishoni mwa msimu wa 2029, unamfanya Clara Luvanga kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania katika historia ya Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake nchini Marekani (NWSL).
Kama sehemu ya uhamisho huo, Washington Spirit italipa ada ya uhamisho kwa klabu yake ya zamani, Al-Nassr FC ya Saudi Arabia, inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia, anaondoka baada ya misimu mitatu yenye mafanikio makubwa.
Tangu alipojiunga na Al-Nassr mwaka 2023, Luvanga aliisaidia klabu hiyo kushinda mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia, pamoja na Kombe la Wanawake la Saudi Arabia, Super Cup ya Wanawake ya Saudi Arabia na ubingwa wa WAFF Women’s Clubs Championship 2026.
Kwa upande wa mafanikio binafsi, Luvanga alitwaa kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia msimu uliopita, baada ya kumaliza akiwa mfungaji bora wa ligi kwa kufunga mabao 24.
Clara anakumbukwa kwa kufunga hat-trick katika fainali ya Super Cup ya Wanawake ya Saudi Arabia mwaka huu.
Wachezaji wengine wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania ni Julietha Singano (FC Juarez, Mexico), Enekia Kasonga (Gallos Femenil, Mexico), Opah Clement (SD Eibar, Hispania), Diana Lucas (Trabzonspo, Uturuki), Noela Luhala (MFA Zalgiris, Lithuania), Hasnath Ubamba (Al Masry, Misri) Violeth Nicholas (Palm Hills SC, Misri) na Aisha Masaka (Brighton & Hove Albion, England).


