Kocha wa Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanaume U20 (Ngorongoro Heroes), Mario Rivera amesema baada ya kufuzu AFCON 2027, sasa akili yao wameihamishia kufanya vizuri ili kukata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2027.
Pamoja na Ngorongoro Heroes kupoteza katika mchezo wa fainali dhidi ya Sudan kwa mikwaju ya penalti 4-3, lakini imefuzu kucheza AFCON 2027 zitakazofanyika nchini Ghana kuanzia mwezi Februari na Machi 2027.
Mario amesema kwa sasa wamefunga ukurasa wa michuano hiyo, wamehamishia mawazo yao kufanya vizuri katika fainali za AFCON ili kufanikiwa kucheza hatua ya nusu fainali ili kukata tiketi ya Kombe la Dunia 2027.
Fainali za Kombe la Dunia 2027 zinatarajiwa kufanyika katika nchi za Azerbaijan na Uzbekistan ambapo timu nne kutoka Afrika zitakazofanya vizuri na kutinga hatua ya nusu fainali za AFCON 2027 zitakata tiketi ya moja kwa moja.
Ngorongoro Heroes katika michuano ya kuwania kufuzu AFCON 2027 kwa Ukanda wa CECAFA, ilianza kwa kuifunga Rwanda mabao 3-0, ikaibamiza Ethiopia 4-0, ikaiondoa Burundi katika nusu fainali kwa mabao 2-0 na ikapoteza kwenye fainali dhidi ya Sudan kwa penalti.


