Ni fainali ya Simba, Azam Kombe la CRDB
Timu ya Azam itacheza na Simba fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kuitoa Young Africans katika hatua ya nusu fainali.
Katika mechi hiyo iliyofanyika Juni 21 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Azam ilishinda mabao 3-2.
Bao la muda wa nyongeza kutoka kwa Jephte Kitambala liliwahakikishia Azam kucheza fainali hiyo Julai 4.
Azam ndiyo walioanza kwa kupata bao kupitia kwa Himid Mao, kabla ya Prince Dube kuizawazishia Young Africans.
Azam walipata bao la pili lililofungwa na beki wa kati Lameck Lawi kabla ya Young Africans kusawazisha tena kupitia kwa nahodha wake Bakari Mwamnyeto, na kufanya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katika dakika 30 za nyongeza, Kitambala aliihakikishia Azam kucheza fainali yao ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kufika katika hatua hiyo na kufungwa na Young Africans.


