TFF yarekebisha Kanuni za Ligi
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho kadhaa kwenye Kanuni za Ligi.
Marekebisho hayo yanayoanza kufanya kazi msimu wa 2026/2027 yalipitishwa katika kikao chake kilichofanyika tarehe 29 Julai jijini Dar es Salaam chini ya Rais Wallace Karia.
Baadhi ya kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni timu itakayogoma kuingia vyumbani (dressing rooms) itakatwa pointi katika msimamo wa Ligi.
Nyingine ni klabu itakayokiuka masharti ya udhamini kwenye Ligi itapigwa faini ya sh. 10,000,000 kwa kila mechi itakayofanya ukiukaji huo.
Ukiukaji wowote wa Taratibu za Mchezo, adhabu yake faini kuanzia sh. 10,000,000 hadi sh. 40,000,000 na/ au kufungiwa mechi zisizozidi tatu au kufungiwa kipindi kisichozidi miezi mitatu.
Katika marekebisho hayo, TFF/TPLB ndiyo itakayosimamia na kuratibu zoezi la kumpata mzabuni wa kuuza tiketi kwa ajili ya mashindano yote yaliyo chini yake.
Vilevile klabu ambayo itashindwa au kukaidi kushiriki sherehe za kukabidhi kikombe cha ubingwa, medali au tuzo nyingine yoyote inayotolewa na TFF/TPLB kutokana na nafasi ya klabu husika kwenye Ligi au shindano ililoshiriki, itatozwa faini isiyopungua sh. 50,000,000 na viongozi wake wakuu watafikishwa kwenye Kamati ya Maadili kwa hatua zaidi.


