Rais Karia aonya kuhusu kanuni
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema marekebisho yaliyofanyika katika kanuni za Ligi na kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF yataanza kutekelezwa rasmi msimu wa 2026/2027.
Hayo ameyasema alipokuwa akizungumza na wanahabari leo Julai 30, 2026 katika makao makuu ya TFF yaliyopo Karume, Dar es Salaam
Rais Karia amesema: Hakuna kanuni mpya ya ligi ambayo haikuwepo katika misimu iliyopita, bali kuna marekebisho kadhaa yaliyofanyika kuelekea msimu mpya wa ligi ambayo yatazidi kuipa thamani ligi yetu.”
Marekebisho ya kanuni yaliyofanyika ni pamoja na matumizi ya vyumba vya kubadilishia (dressing rooms) katika uwanja husika wa mechi na endapo kanuni hii itakiukwa timu husika itakatwa pointi katika msimamo wa Ligi.
Matumizi ya teknolojia ya Football Video Support (FVS) itakayowasadia makocha na wahusika wengine kuomba marejeo ya matukio mbalimbali wakati wa mechi itakayoanza msimu wa 2026/2027.
Kutofuata taratibu za mchezo timu itaadhibiwa kwafaini kuanzia sh. 10,000,000 hadi sh. 40,000,000 au kufungiwa mechi zisizopungua 3 au vyote kwa pamoja.
Mbali na hayo, Rais Karia aligusia pia kanuni ya wachezaji wa kigeni watakaosajiliwa kucheza katika Ligi ya Tanzania lazima wawe wanacheza katika ligi kuu ya nchi anayotokea, lakini pia awe mchezaji anayetumikia timu ya taifa lake kipindi anasajiliwa na kusisitiza kuwa kanuni hii itasimamiwa kikamilifu na TFF na Bodi ya Ligi.


