Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefanya uteuzi la Katibu Mkuu mpya, pamoja na kufanya mabadiliko katika baadhi ya Kurugenzi zake.
Mabadiliko hayo yametangazwa leo Septemba 28, 2026 baada ya kikao cha Kamati Utendaji ya TFF, chini ya Rais wake, Wallace Karia kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika uteuzi huo, Evance Mgeusa amekuwa Katibu Mkuu mpya wa TFF akijaza nafasi ya Oscar Milambo ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Mgeusa alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NIOREFA).

Pia Milambo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu, wakati Mustapha Yusuph anakuwa Mkurugenzi mpya wa Fedha.
Katika mabadiliko hayo, Kurugenzi ya Sheria, Habari na Masoko imegawanywa na kuwa Kurugenzi tatu tofauti, ambapo walioteuliwa kuongoza Kurugenzi hizo ni Hassan Njama (Biashara na Masoko), Boniface Wambura (Sheria) na Cliford Mario Ndimbo (Habari na Mawasiliano).


