Timu nne za ligi kuu ya Wanawake WPL zatunishiana misuli kuelekea michezo miwili ya nusu Fainali Ngao ya jamii 2026 septemba 30.

    Michezo hiyo itakayopigwa uwanja wa KMC, Mwenge Dar es salaam itazikutanisha timu za JKT Queens na Mashujaa Queens majira ya saa 9:00 alasiri, huku watani wa jadi Simba Queens na Yanga Princess wakimalizia burudani hiyo ya soka la wanawake kwa mchezo wa nusu fainali ya pili majira ya saa 12:00 jioni.

    Wakizungumza wakati wa mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Septemba 29, 2026 makocha hao wote walionyesha utayari wao huku kila mmoja akivutia kamba upande wake kwa kujinasibu kuwa na timu bora zaidi ya kiushindani.

    “Tumejipanga vizuri, niwaombe mashabiki wa Mashujaa Queens wajekutupatia sapoti ili waone pia usajili mpya wa kikosi chao kuelekea msimu ujao wa ligi kuu” alisema kocha Rajabu Bwamkuu wa Mashujaa Queens.

    “Mashabiki zetu wawe tayari kupokea raha, hatuna shaka na wachezaji waliopo kwani tunawachezaji wengi bora” alisema kocha Juma Kessy wa JKT Queens.

    “Mashabiki zetu wasiache kutusapoti licha ya kutopata matokeo mazuri mbele ya Simba Queens kwenye michezo iliyopita hivi karibuni, tumejipanga vizuri hivi sasa hivyo wapinzani wetu pia wasije na matokeo” alisema kocha Edna Lema wa Yanga Princess.

    “Simba Queens tunahitaji Ubingwa wa Ngao ya jamii, tunakwenda kwenye ushindani wao wanajua wanachokitaka na sisi pia tunajua malengo yetu kikubwa hatuhitaji kufungwa na Yanga Princess “ alisema Musa Mgosi kocha wa Simba Queens.

    Ikumbukwe mechi zote hizo ambazo ni tafsiri ya kukata utepe wa msimu mwingine wa ligi kuu ya wanawake (WPL 2026-2027) hazitakuwa na kiingilio.

    Share.