Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

BMT yatoa tuzo kwa wanamichezo nchini

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limetoa tuzo kwa wanamichezo Bora nchini katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Lengo la tuzo hizo ni kutambua na kuthamini mchango wa wanamichezo wanaofanya vizuri ngazi ya taifa na kimataifa lakini pia kutambua mchango wa wadau mbalimbali wanaochangia kupeleka mbele maendeleo ya michezo nchini.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa tuzo hizo  mgeni rasmi  Waziri wa utamaduni sanaa na michezo Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana alisema “serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia suluhu Hassan imedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya michezo hivyo wadau wa michezo wakae tayari”.

Hata hivyo Waziri Chana hakuacha kugusia mafanikio makubwa katika soka ikiwa ni pamoja na  na ligi ya Tanzania kuwa ligi bora namba tano barani Afrika. Timu ya taifa ya wanawake ya Serengeti Girls  kufanya vizuri kimataifa katika mashindano ya  kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 17, na timu ya Tembo warriors kufika hatua ya robo fainali  katika mashindano ya Dunia.

Leodgar Tenga Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa ( BMT)  alisema ” Baraza litaendelea kutekeleza programu mbalimbali zenye lengo la kutambua jitihada na vipaji vya wanamichezo mbalimbali ili kutoa hamasa Kwa wanamichezo wengine.

Tuzo mbalimbali zilitolewa ambapo tuzo ya heshima ilikwenda kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya Michezo.Tuzo ya timu bora ya mpira wa miguu iliyofanya vizuri kimataifa ilienda Kwa timu ya Serengeti Girls wakati Simba Queens ikinyakua Tuzo ya timu bora ya  mpira wa miguu na Tembo warriors nao wakatwa tuzo ya timu bora  ya walemavu iliyofanya vizuri kimataifa Kwa upande wa soka.

Clara Luvanga alitwaa Tuzo mbili ya mwanamichezo bora wa kike katika mchezo wa mpira wa miguu na mwanamichezo bora wa kike wa jumla huku Aishi Manula golikipa wa klabu ya Simba SC akitwaa tuzo ya mwanamichezo bora wa kiume katika soka akiwabwaga Shomari Kapombe na Mohammed Hussein. Benki ya NBC na Azam TV nao ni miongoni mwa wadhamini waliopata tuzo katika usiku wa mwanamichezo.

Tuzo hizo zilihudhuriwa na Waziri wa utamaduni sanaa na michezo aliyeambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, Katibu mkuu wa wizara hiyo Saidi Yakubu.Wengine ni wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania,  Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia na Marais wengine wa vyama vya michezo, wanamichezo na wadau mbalimbali wa michezo kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

 

 

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.