Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) ipo tayari kwa mchezo wake wa mkondo wa kwanza wa kufuzu Olimpiki Los Angeles 2028 dhidi ya Botswana utakaochezwa kesho Oktoba 9, 2026 jijini Gaborone nchini Botswana.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime amesema ana matumaini ya kufanya vizuri kulingana na maandalizi waliyoyafanya kuelekea mchezo huo.
Alisema wanaufahamu ugumu wa wapinzani wao hivyo wanakwenda kwa kuwaheshimu licha ya kuwa na rekodi ya kupata ushindi ugenini dhidi yao wa bao 1-0 kwenye mchezo wa nyuma.
“Tuna faida ya kuwa na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje, uzoefu wao utatusaidia katika mchezo huo,” alisema Shime.
Aliongeza kuwa wachezaji wana morali ya kutosha kupambana kutokana na uzoefu walioupata hivi karibuni katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026).
Baada ya mchezo wa kesho Twiga Stars watarudiana na Botswana Oktoba 13, 2026, jijini Dar es Salaam.


