Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe  (Mb) leo tarehe 3 Aprili 2017 ameshiriki kwenye zoezi la kuwaaga na kuwapatia bendera ya Taifa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys).

Mhe. Mwakyembe amewaasa vijana wa Serengeti kuliwakilisha vyema Taifa kwenye michuano ya AFCON wanayotarajia kwenda kushiriki hivi karibuni.

Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys, kesho Jumatatu itapambana na Black Starlets ya Ghana kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni, Serengeti Boys itautumia kama ni ishara ya kuwaaga mamilioni ya Watanzania kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amezipa kongore timu za JKT Oljoro ya Arusha, Mawenzi ya Morogoro na Transit Camp ya Shinyanga kwa kufanikiwa kupanda daraja baada ya kufanya vema kwenye hatua ya Nne Bora (Play off) iliyofikia kikomo jana Aprili mosi, mwaka huu.

Katika salamu zake za pongezi, Rais Malinzi amezitaka timu hizo sasa kujiimarisha katika nyanja za usajili na maandalizi mengine ili kuwa timu za ushindani katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambako watashiriki kuanzia msimu mpya utakaoanza Julai, mwaa huu.

Kamati ya Rufani za Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetupa rufaa Saleh Saleh maarufu kama Ndonga aliyelalamikia kuhusu uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kadhalika kumlalamikia Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Almas Kasongo akitaka ang’olewe kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa sasa.

Pia katika uamuzi wake huo Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya TFF, imesema kila upande ubebe gharama zake kwani rufaa hyo haina sababu za msingi za kusitisha mchakato wa usaili au kuweza kumuengua Kasongo katika kinyang’anyiro cha kugombea uongozi DRFA.

Baada ya kusimama kwa muda wa takribani wiki tatu kupisha michuano mbalimbali ya kimataifa kwa ngazi ya timu ya taifa na klabu, kadhalika michuano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inarejea tena kesho Jumamosi kwa michezo miwili.

Michezo ya kesho Jumamosi Aprili mosi, mwaka huu itakuwa kati ya Mabingwa watetezi wa VPL, Young Africans na Azam - mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Mbeya City na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Mechi zote za Jumamosi, zitafanyika saa 10.00 jioni.