Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana tarehe 18/01/2017 katika ofisi za TFF pamoja na mambo mengine pia ilijadili suala la uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA).

 

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilizuia mchakato huo usiendelee kwa barua ya tarehe 19/12/2016 yenye kumbukumbu Na TFF/ADM/LM.184/2016, kwa sababu ya rufaa iliyowasilishwa katika kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.

Raundi ya tano ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam 2016/17 (Azam Sports Federation Cup - ASFC), utaanza Jamamosi Januari 21, 2017 kwa timu za Majimaji na Mighty Elephant za Songea kucheza kwenye Uwanja Majimaji mjini Songea.

Ratiba ya ASFC inaonesha kwamba timu za Alliance na Mbao za Mwanza zitacheza pia keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wakati Young Africans itacheza na Ashanti United kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya soka ya FIFA kwa miaka minne ijayo. Uteuzi huo unaanza mwaka huu 2017 hadi 2021.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Januari 18, 2017 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Fatma Samoura inasema: “Tuna faraja kukufahamisha kuwa umeteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya FIFA. Tunachukua nafasi hii kukupongeza kwa uteuzi huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limepitisha ombi la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa CAF. Katika kikao chake cha Kamati ya Utendaji kilichoketi Januari 12, mwaka huu kiliamua kupitisha ombi hilo kuwa moja ya ajenda za Mkutano Mkuu wa CAF utakaofanyika Machi 16, 2017 huko Addis Ababa, Ethiopia.

Hivyo sasa Mkutano Mkuu huo utapiga kura na kama Zanzibar itapata idadi ya kura theluthi mbili yaani 2/3 ya wanachama wote, itatangazwa kuwa mwanachama mpya kamili wa CAF ambako atakuwa na haki mbalimbali za kama mwanachama.

Wakati Ligi Kuu soka ya Wanawake ikitarajiwa kuendelea kesho Ijumaa Januari 20, 2017 kwa michezo mitano, wachezaji 19 kati 25 bora walioteuliwa katika mradi wa kuibuka na kukuza vipaji vya soka wa Airtel (Airtel Rising Stars), wametawala katika klabu zinazoshiriki michuano hiyo, inayoendelea.

Wachezaji hao wanaocheza kwa mafanikio makubwa ni Agatha Joel, Fabiola Fabian, Eva Jackson, Zainabu Mrisho, Fumu Mohamed, Stella Wilbert, Christina Samwel, Shamimu Hamisi, Oppa Msolidi na Yustina Mboje ambao wamesajiliwa na Klabu ya Evergreen ya Temeke, Dar es Salaam.